Mabadiliko ya tabianchi huathiri upatikaniaji wa maji
Upatikanaji wa maji safi kwa ajili ya watoto uko hatarini
Kupungua kwa vyanzo vya maji safi kote ulimwenguni ni tishio kubwa kwa afya na maisha. Inakadiriwa kuwa hadi mwaka 2020, mabadiliko ya tabia ya nchi yatawaweka hatarini takribani watu milioni 75 barani Afrika peke yake kwa sababu ya upungufu wa maji.
Maji safi ni muhimu kwa maisha, afya bora na njia za kujipatia riziki. Mabadiliko ya tabia ya nchi huenda yakasababisha kuongezeka kwa ukame, mafuriko na hata kina cha bahari, ambapo mambo yote haya yatafanya upatikanaji wa maji safi na salama kuwa mgumu zaidi. Kuongezeka kwa uchafuzi wa maji, matumizi ya kupita kiasi ya maji yaliyo ardhini na uharibifu wa vyanzo vya maji unaongeza makali ya hali ambayo tayari ni ngumu. Wakati huo huo, uchafuzi unaosababishwa na viwanda, kilimo na usimamizi mbaya unatishia vyanzo vya maji vilivyokuwa salama hapo kabla.
Pale ambapo ni kiasi kidogo tu cha maji safi kinapatikana, kuna uwezekano watu wakabana matumizi yake ili yawe ya kunywa tu na hivyo kutumia maji kidogo sana ili kunawa mikono na kujiweka safi. Matumizi ya maji machafu na mazingira machafu yanaweza kusababisha magonjwa.
Zaidi ya hayo, upungufu wa maji unaweza kusababisha migogoro, kwani wengine watataka kulinda vyanzo vyao, na watu wengi zaidi kuhama, kwani watu wanahamahama na kwenda paliko na maji.
Ufumbuzi ni kuwa na usimamizi mzuri wa maji na usafi. Ni muhimu kuendeleza njia na teknolojia mpya ili kutumia maji kwa usalama na kulinda rasilimali maji. Suala la kusafisha maji machafu ili kuyatumia upya huenda likawa na gharama ndogo, lakini pia la lazima.