Mabadiliko ya tabianchi yanachochea majanga ya asili
Watoto wako katika hatari kubwa zaidi wakati wa majanga ya asili
Katika nusu ya kwanza ya karne ya 20, wastani wa utokeaji majanga ulikuwa ni 12 kwa mwaka, idadi hiyo iliongezeka katika viwango vya kutisha kwa kufika wastani wa majanga 350 mwaka 2004.
Kuongezeka kwa ukali wa matukio ya hali mbaya ya hewa kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi—kama vile ukame, mafuriko na vimbunga vya nchi kavu na baharini—kunawaweka watu katika hatari, huku mara nyingi yakiharibu mahali wanakoishi na kufanya kazi watu na kusababisha uharibifu wa mazao, kuchafua vyanzo vya maji na hata kutenganisha familia.
Ingawa majanga ya asili humletea madhira makubwa yanapompata mtu, watoto ndio walio katika hatari zaidi, hasa kwa sababu ya udogo wa maumbo yao na uwezo mdogo wa kujilinda wenyewe.
Watoto wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupoteza maisha wakati wa majanga ya asili au kupatwa na utapiamlo, majeraha au magonjwa mara baada ya janga. Majanga ya asili yanaweza kuwafanya watoto wakimbie makwao—au hata nchi zao. Wanaweza kuingia katika hali ya uyatima au kutengwa na familia zao, na hapo wanaweza kugeuzwa asusa na watu wazima wanaojitafutia faida.
Jitihada za kupunguza hatari hazina budi kubuniwa ili kutoa elimu kwa familia na watoto kuhusu njia rahisi na vitendo wanavyoweza kuvifanya ili kulinda uhai na mali yao pale majanga ya asili yanapotokea. Programu zenye tija za utoaji elimu mashuleni, nyumbani na katika jamii zinaweza kuleta utamaduni wa kujilinda na uwezeshaji.