Mabadliko ya tabianchi huathiri upatikanaji wa chakula
Mabadliko ya tabia ya nchi hutishia uhakika wa kupata chakula
Uhakika wa upatikanaji chakula huathiriwa na mabadiliko ya tabia ya nchi kwani ukame, mabadiliko ya vizio vya joto, mioto ya nyikani, matukio ya hali mbaya ya hewa, wadudu waharibifu wa mazao, magonjwa na mafuriko yanaweza kuharibu mazao ya chakula. Jambo hili linaongeza matatizo katika mgogoro ambao tayari upo ulimwenguni wa chakula, kwani chakula kikuu kama vile mpunga, ngano na mahindi vinaathirika.
Kuongezeka kwa tatizo la utapiamlo kunaweka afya na maisha ya wanawake na watoto katika hatari na kuongeza mzigo kwa watu wanaoishi na VVU wanaotumia dawa za kupunguza makali ya virusi, kwani mlo kamili kwao ni muhimu ili tiba yao ifanikiwe.
Wanasayansi wanabashiri kwamba ongezeko la joto na mabadiliko ya mienendo ya mvua huenda yakaathiri uzalishaji hasa katika maeneo yenye matatizo. Katika nchi zinazoendelea, suala hili litawaathiri mamia ya mamilioni ya watu ambao hawatakuwa na uwezo wa kuzalisha wala kununua chakula cha kutosha.
Zaidi ya hayo, mabadiliko ya utegemeano wa viumbe-hai yanayotokana na tabia ya nchi yanaongeza ugumu katika kutafuta vyanzo vya chakula maporini, hasa kwa sababu maarifa ya watu kuhusu wapi wanaweza kwenda kuwinda, kuvua samaki au kuokota chakula na mimea yamepungua sana.
Lakini jitihada za kawaida tu zinaweza kuleta matunda makubwa. Katika Kijiji cha Alikinkin, huko Niger, bustani za jamii ni visiwa vya uzuri na chanzo cha chakula ambapo huwasaidia watoto kuepuka madhara makubwa ya mgogoro wa lishe.