Matokeo ya mabadiliko ya tabianchi ni yapi?
Maisha yetu yanaathiriwa vipi na mabadiliko ya tabia ya nchi?
Ingawa nchi zilizoendelea na zile zinazokua haraka ndiyo watumiaji wakuu wa nishati kama vile makaa ya mawe na gesi na rasilimali nyingine, madhara ya mabadiliko ya tabia ya nchi mara nyingi yanazikumba zaidi nchi maskini, ambako watu wengi tayari wana upungufu wa chakula na maji huku wakikabiliwa na maradhi kama vile kipindupindu, ambacho husambaa kwa kasi zaidi kunapokuwa na majanga ya asili kama vile mafuriko au tufani na hivyo kuongeza madhira kwa miundombinu dhaifu ya maji na mifumo ya kufanyia usafi.
Mabadiliko ya tabia ya nchi yanaathiri nyanja mbalimbali za maisha yetu kiasi kamba sasa limevuka kutoka kuwa suala la ‘kimazingira’ kufikia kuwa jambo linalohitaji ujuzi wa kila mmoja ili kuleta maendeleo endelevu, uhakika wa upatikanaji nishati, na afya bora na ustawi wa watoto.
Hii hapa ni baadhi ya mifano: ● Kupata maji safi na salama ni suala muhimu sana kwa uhai, afya na maisha bora. Mabadiliko ya tabia ya nchi yanatarajiwa kusababisha ukame, mafuriko na kuongezeka kwa kina cha bahari, ambapo mambo yote haya yatafanya upatikanaji wa maji safi na salama kuwa mgumu zaidi. ● Suala la uhakika wa kupata chakula linaathiriwa na mabadiliko ya tabia ya nchi. Ukame, kupanda na kushuka kwa joto, mioto ya nyikani, matukio ya hali mbaya ya hewa, wadudu waharibuo mazao, magonjwa na mafuriko yanaweza kuharibu mazao ya chakula. Tatizo la utapiamlo linalozidi kukomaa huweka afya na uhai wa wanawake na watoto katika hatari na kuongeza mzigo kwa watu wanaoishi na VVU wanaopata dawa za kupunguza makali ya virusi, maana kwa watu hawa lishe ya uhakika ni muhimu ili tiba yao ifanikiwe. ● Matokeo ya wazi ya mabadiliko ya tabia ya nchi ni familia kuhama na kwenda uhamishoni, jambo ambalo daima huwa na athari mbaya kwa watoto. Kutokana na hali hizi, watoto wanakuwa katika hatari zaidi ya kufanyiwa ukatili na hata kuuzwa. Mara baada ya majanga kutokea, watoto wanaweza kuondolewa mashuleni ili wafanye vibarua kusaidia familia zao kuhimili makali ya maisha. ● Magonjwa kama vile malaria, homa ya denge na homa yabisi ambayo yanasababishwa na wadudu, na yanachochewa na mabadiliko ya viwango vya joto maana wadudu wanazaliana hata katika maeneo ambayo hapo awali hawakuweza. Hivi sasa wadudu hawa wanapatikana hata katika nchi za kaskazini ambako kulikuwa baridi mno kwao kuzaliana. ● Kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa kunakosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi nako huwaweka watu katika hatari, ambapo mara nyingi huharibu makazi yao na kuharibu mazao yao, kuchafua vyanzo vyao vya maji na kutenganisha familia. ● Moshi na uchafu unaotokana na kuungua kwa makaa ya mawe na mafuta katika nyumba, mabasi, magari na viwandani yote yanaongeza utoaji wa gesi inayoharibu anga linalozuia miali ya jua, wakati huohuo ukichafua hewa tunayovuta na kusababisha matatizo ya afya.